#UsalamaWaMtandaoni: Ingia Mwaka Mpya 2026 Kibabe Ukiwa na Mbinu Hizi 51 za Kujilinda Mtandaoni
Nywila (passwords)
1 Epuka kutumia nywila ambayo ni rahisi kutabirika
2 Epuka nywila inayotokana na taarifa zako kwa mfano tarehe yako ya kuzaliwa
3 Tumia kundi la maneno angalau manne ambayo hayahusiani.
4 Tumia mchanganyiko wa herufi kubwa na ndogo za tarakimu maalum (mfano @$%) sio chini ya kumi
5 Tumia meneja wa nywila (password manager)
6 Tumia uthibitisho wa hatua mbili (two-factor authentication)
7 Usimpatie nywila yako mtu yeyote yule hata kama ni nani
8 Usiandike nywila yako mahala popote pale, au kuihifadhi mahala inaweza kuonekana
9 Badili nywila yako mara kwa mara
10 Kamwe usitumie nywila yako zaidi ya mara moja. Nywila zako shurti ziwe za kipekee na zisizohusiana
Kuvinjari mtandaoni (web browsing)
11 Kamwe usibonyeze kiungo (link) usicho na hakika nacho
12 Hakiki anwani ya tovuti unayotembelea kujiridhisha kuwa ni hiyo kweli unayotaka kuitembelea
13 Hakikisha tovuti unayotembelea inaanza na https kwenye anwani. Kinyume cha hivyo, tovuti hiyo sio salama
14 Hakikisha tovuti unayotembelea ila alama ya funguo kabla ya anwani
15 Epuka tovuti yenye matangazo yanayohadaa kama ni halali. Kwa kifupi, kamwe usipakue (don’t download) kitu usicho na hakika nacho.
16 Mtandao una matabaka makuu matatu: la kwanza ni “surface web”, la pili ni “deep web”, na la tatu ni “dark web”. Kwa kifupi, tabaka la “dark web” ni hatari, limejaa utapeli na shughuli zilizo kinyume cha sheria. Epuka tabaka hilo.
17 Hakikisha unapakua (download) tu kitu ambacho chanzo chake ni cha kuaminika. Na hata ukishapakua, kwa mfano faili, ni muhimu kuhakiki usalama (scan) kwa kutumia programu tumizi ya kupambana na virusi (anti-virus software)
Mitandao ya kijamii (social media)
18 Kila unachoweka mtandaoni hukaa milele, kwahiyo ni vema uweke mtandaoni kile tu una amani nacho kuwepo huko.
19 Hakiki kwa kina vipimo (settings) vya usalama wako katika mtandao wa kijamii husika ili ufahamu kitu gani kinaonekana hadharani (kwa mfano tarehe yako ya kuzaliwa, namba ya simu,nk)
20 Kamwe usimruhusu mtu yeyote yule kutumia akaunti yako ya mtandao wa kijamii, na usithubutu kuingia kwenye akaunti yako ya mtandao wa kijamii wakati unatumia kompyuta inayotumiwa na watu wengi.
21 Mitandao ya kijamii imesheheni utapeli na uongo. Kuwa makini. Kama kitu kinaonekana kizuri kupita ukweli basi si kweli.
22 Usisambaze vitu ovyo kwenye mitandao ya kijamii kwani hujui nani anawinda taarifa zako na walionazo wanazifanyia nini (unaweza kujidanganya kuwa “mie sio mtu hatari kama Jasusi, kwahiyo hakuna wa kuniwinda”)
23 Shirikisha (share) taarifa zile tu ambazo mhusika amekupa idhini. Wadhani ni sahihi kuweka mtandaoni picha za mwanao?
Programu tumizi ya kupambana na virusi vya kompyuta (antivirus).
24 Kila mfumo wa kompyuta una uwezekano wa kushambuliwa na virusi
25 Kama unatumia kompyuta yenye Windows, huhitaji kuingia gharama kununua programu tumizi ya kupambana na virusi vya kompyuta kwani kuna “Windows Security”
26 Epuka kupakua programu usizo na uhakika nazo sambamba na kuepuka kufungua viambatanishi katika baruapepe (email attachment) kutoka kwa watu usiowafahamu
27 Jielimishe kuhusu virusi, programu tumizi za dhamira ovu (malicious software aka malware) na programu tumizi zinazorekodi kila unavyobonyeza tarakimu kwenye kompyuta (keyloggers)
28 Njia kubwa zaidi ya kusafisha kompyuta yako ni kufuta kila kitu
Data
29 Tumia njia za kuweka data zako salama (encryption) na kamwe usimpatie mtu funguo ya njia husika (encryption key)
30 Usihifadhi data kwenye mfumo wa “cloud”, badala yake ondoa kabisa katika mtandao
31 Vifaa vya kuhifadhia data vinaweza kuibiwa, kwahiyo kuwa makini kuhusu nini unahifadhi humo.
32 Ukiamua kufuta data kwenye chombo unachotumia, tumia njia za kuhakiki kuwa data zimefutwa kabisa.
33 Ukinunua kompyuta iliyotumika, futa data zote kabla ya kuanza kuitumia.
34 Hifadhi data zako angalau kopi tatu katika vyombo tofauti vya kuhifadhi data.
Baruapepe (email)
35 Anwani ya mtuma baruapepe inaweza kuwa feki ili kumhadaa mtumiwa. Jiridhishe.
36 Unamjua aliyekutumia baruapepe? Ulitarajia baruapepe husika? Kama majibu ni hapana, usiifungue bali ifute mara moja.
37 Kama baruapepe inakuagiza kubonyeza kiungo (click link) au kufungua kiambatanisho (attachment) ambacho kinatia shaka, amini “machale” yako, usifungue.
38 Ukitumiwa baruapepe inayokutaka utume taarifa zako nyeti, usifanye hivyo. Sio benki wala taasisi yoyote inayohusiana na taarifa zako nyeti itakayokuandikia baruapepe kuomba taarifa zako.
39 Ukipata baruapepe ambayo mtumaji anajaribu kukuonyesha kama ni dharura, huenda ni utapeli. Jiridhishe kwanza
40 Yule ndugu wa tajiri maarufu au mtawala aliyefariki, anayetaka kuingiza fedha kwenye akaunti yako ni tapeli. Haiwezekani kamwe mtu asiyekujua kutaka kukutumia japo shilingi mia achilia mbali hayo mamilioni ya dola.
41 Sio kila baruapepe inayoingia kwenye “boksi kuu” (inbox) ni salama. Vipimo vya kuchuja baruapepe feki (spam filters) sio vya kuaminika sana.
Programu tumizi (software)
42 Sasisha (update) programu tumizi kwenye kompyuta yako.
43 Sasisha mfumo wa uendeshaji kompyuta (operating system) yako
44 Kama una programu tumizi huihitaji tena kwenye kompyuta yako, iondoe (uninstall)
45 Usiingize viendelezi vya vivinjari (browser extensions) ambavyo huna hakika navyo.
Simu janja (smartphones)
46 Unaposakinisha (install) programu tumizi (app) kwenye simu janja yako, angalia ruhusa (permissions) zinazoombwa, kuwa makini na maombi ya ruhusa (access permissions) kuhusu kamera, kipaza-sauti (microphone) na mahali (location)
47 Sanikisha programu tumizi kutoka maduka rasmi ya programu tumizi (app stores), na hata hapo pia wapaswa kuwa makini.
48 Kamwe usitume taarifa nyeti endapo unatumia “WiFi” ya matumizi kwa kila mtu (public WiFi)
49 Linda simu janja yako na kwa kutumia njia za ulinzi kama tarakimu za siri (PIN), alama za vidole, nk
50 Iga njia unazotumia kwenye usalama wa kompyuta yako na uzitumie kulinda usalama wa simu janja yako
51 Kaa na simu yako badala ya kuiacha na mtu mwingine au mahala ambapo mtu mwingine anaweza kuihujumu.




